Uvimbe kwenye mayai-Ovarian cyst

uvimbe kwenye mayai ya mwanamke

Polycystic ovary syndrome kwa kifupi PCOS ama uvimbe kwenye mayai. Ni kisababishi namba moja kwa ugumba kwa wanawake wengi duniani kote. Tatizo hili ni ugonjwa angamivu wa kimyakimya, yaani unakutafuna kimyakimya bila kufahamu mpaka pale tatizo linapokuwa kubwa.

Huwaathiri zaidi wanawake waliopo kwenye umri wa kuzaa miaka 18 mpaka 35. Habari njema ni kwamba kuna njia mbadala kutibu tatizo lako la PCOS ambapo inaanzia katika kubalansi homoni zako za kike. PCOS ni mkusanyiko wa vimbe ndogondogo nyingi tunazoziita ovarian cyst.

Uvimbe kwenye mayai(PCOS) ni Kitu gani

Uvimbe kwenye mayai ya mwanamke (ovary) hutokana na mkusanyiko wa majimaji yanayozungukwa na kuta nyembamba ndani ya mayai ya mwanamke. Uvimbe huu ambao hupatikana ndani ya mayai ya mwanamke ndio unaojulikana kama ovarian cyst.

Wakati fulani mifuko midogo hujitengeneza juu ya yai lililokomaa. Kimfuko hichi hupotea pale yai linapotolewa kwenye hedhi. Inotokea yai limekomaa na halijatolewa basi kimfuko hichi hujifunga na kuwa na maji ndani yake. Kimfuko hichi tunakiita ovarian cyst na vinapokuwa vingi tunaviita polycystic.

Kwahiyo Polycystic ovarian syndrome ni mkusanyiko wa dalili zinazoambatana na uwepo wa vimbe hizi ndogo ndogo(cysts) kwenye mifuko ya mayai ya mwanamke.

Uvimbe huu unaweza kumtokea mwanamke wa umri wowote ingawa mara nyingi huonekana kwa wanawake waliofikia menopause.

Mayai ya mwanamke

Kwa kawaida mwanamke anakuwa na viwanda viwili vya kuzalisha mayai katika mwili wake. Yai moja upande wa kulia na yai jingine upande wa kushoto. Mayai haya hupatikana pembezoni mwa mfuko wa uzazi (uterus).

Mifuko ya mayai huanza kuzalisha mayai ya uzazi yanayojulikana kama ovum. Ambapo mayai hayo ya uzazi hukua ndani ya mayai ya mwanamke (ovary) kwa kuchochewa na baadhi ya homoni.

Katikati ya mwezi, siku ya kumi na nne, saa 24-36 baada ya kiwango cha kichocheo aina ya luteinizing hormone kuwa juu, mayai ya uzazi hutolewa katika kila ovari na hii ndio hujulikana kama ovulation au upevukaji mayai. Mayai haya ya uzazi huishi kwa saa chache hadi saa 24 ikiwa hayatorutubishwa na mbegu za kiume.

Hedhi

Mabaki ya mfuko wa mayai ya uzazi yanayojulikana kama follicle ndani ya ovari, hugeuka na kuwa corpus luteum ambao huhusika na utoaji wa kichocheo au homoni aina ya progesterone kwa wingi.

Homoni hii ya progesterone ndio inayosababisha mfuko wa uzazi kujiandaa kwa kujikita yai (implantation) lililorutubishwa kwa mbegu ya kiume ndani ya mfuko wa uzazi kwa kuongeza unene kwenye kuta zake.

Yai hili husafiri hadi kwenye mfuko wa uzazi ambako hukua na kuwa mtoto. Kama upachikwaji wa yai liliorutubishwa hautafanyika, basi ndani ya wiki mbili, corpus luteum huanza kusinyaa na kupotea na kusababisha kushuka kwa kiwango cha homoni aina ya progesterone na estrogen.

Kushuka kwa kiwango cha vichocheo hivi ndio husababisha mfuko wa uzazi kuanza kutoa mabaki ya kuta zake pamoja na yai la uzazi na ndipo pale mwanamke anapoanza kuona siku zake za hedhi(kutokwa na damu ukeni).

Aina za uvimbe kwenye mayai ya mwanamke(ovarian cyst)

Kuna aina nyingi za uvimbe kwenye mayai ya mwanamke ila  aina hizi saba ndio huonekana sana kwa wanawake wengi.

1.Aina ya kwanza ni Follicular cyst ambayo uvimbe hutokea wakati ovulation isipotokea au baada ya corpus luteum kuanza kusinyaa na kupotea yenyewe baada ya kutopachikwa kwa yai kwenye kuta za mfuko wa kizazi.

Uvimbe huu unakuwa na wastani wa inchi 2.3 kwa upana. Upasukaji wa uvimbe huu husababisha maumivu makali sana katikati ya mzunguko wa hedhi yaani siku ya ovulation.

Kwa kawaida uvimbe huu hauna dalili zozote na hupotea wenyewe baada ya miezi kadhaa.

2.Aina ya pili ni Corpus Luteum cyst– ambao ni uvimbe unaosababishwa na kutopachikwa kwa yai la uzazi lililorutubishwa na mbegu ya kiume kwenye mfuko wa kizazi. Kwa kawaida corpus luteum husinyaa na kupotea yenyewe, au wakati mwengine inaweza ikajaa maji na hivyo kusababisha uvimbe. Uvimbe huu huonekana kwenye upande mmoja (kushoto au kulia) wa mwanamke na hauna dalili zozote zile.

3.Uvimbe wa tatu ni  Hemorrhagic cyst- Uvimbe huu hutokea wakati kukiwa na uvujaji wa damu ndani ya uvimbe wa aina yoyote ule ambao umeshajitengeneza tayari. Huambatana na maumivu makali kwenye upande mmoja wa ubavu wa mwanamke.

4.Uvimbe mwingine ni Dermoid cyst– ambao sio saratani na pia hujulikana kama mature cystic teratoma, huathiri wanawake wadogo walio katika umri wa kushika mimba na huweza kukua na kufikia inchi 6 kwa upana na ndani huweza kuwa na mchanganyiko wa nywele, mfupa, mafuta na cartilage. 

Uvimbe wa aina hii huweza kuwa mkubwa zaidi au kujizungusha na hivyo kuathiri usambazaji wa damu kwenda kwenye uvimbe huu na hivyo kusababisha maumivu makali sana maeneo ya tumboni.

5.Aina nyingine ni polycysitic appearing cyst- ambao unakuwa mkubwa sana na huwa umezungukwa na vijivimbe vingine vidogo vidogo na huonekana hata kwa wanawake wenye afya njema au wale wenye matatizo ya homoni.

6.Aina ya sita ya uvimbe ni Cystedenoma-Ni aina ya uvimbe unaotokana kwenye tishu za ovari na hujazwa na majimaji yenye kuvutika. Uvimbe wa aina hii huweza kuwa mkubwa sana hata kufikia inchi 12 au zaidi kwa upana.

7.Aina ya mwisho ya uvimbe unaowapata wanawake ni endometriomas /Endometrial.

Nini husababisha uvimbe kwenye mayai

Hapa chini ni sababu hatarishi zinapolekea tatizo la uvimbe kwenye mayai ya mwanamke.

 • Historia ya awali ya ovarian cyst. Kwa wanawake ambao wazazi wao au watu wao wa karibu wamekuwa wakisumbuliwa na ugonjwa huo kuna uwezekano mkubwa nao wakapatwa na tatizo hilo.
 • Sababu nyingine inayoweza kuletekeza uvimbe kwenye mayai ya mwanamke ni kuwa na mzunguko wa hedhi usiokuwa na mpangilio maalum.
 • Kihatarishi kingine ni kuwa na mafuta mengi kwenye sehemu ya juu ya mwili na hii ni kwa wenye uzito mkubwa na kitambi
 • Ugumba na kuvunja ungo mapema ni sababu nyingine ambapo mtoto wa kike hasa anayevunja ungo akiwa na miaka 11 au chini ya hapo huweza kupatwa na uvimbe kwenye mayai yake.

Dalili za kuwa una uvimbe kwenye mayai

 • Maumivu makali ya tumbo, ambayo hayana mwanzo maalum na yanayochoma, ambapo maumivu hayo yanaweza yakawa yanakuja na kupotea au yakawepo moja kwa moja.
 • Kuhisi tumbo kuwa zito, kujaa au kuvimba
 • Maumivu kwenye matiti na hedhi isiyokuwa na mpangilio maalum
 • Maumivu ya muda mrefu kwenye nyonga wakati wa hedhi na ambayo huweza kuhisiwa sehemu ya chini mgongoni, maumivu haya yanaweza kuanza muda mfupi tu baada ya kuanza hedhi, wakati wa hedhi au mwisho wa hedhi.
 • Maumivu ya nyonga baada ya kufanya kazi ngumu, mazoezi au baada ya tendo la ndoa
 • Kuhisi kichefuchefu, kutapika na kutokwa na matone ya damu ukeni.
 • Dalili nyingine ni ugumba na kuhisi uchovu, mabadiliko ya haja ndogo yaani kukojoa mara kwa mara, kujikojolea au kushindwa kutoa mkojo wote kutoka kwenye kibofu cha mkojo wakati wa kupata haja ndogo.

Vipimo

Mgonjwa kufanyiwa endovaginal ultrasound. Ambayo hufanywa kwa kuingiza mpira maalum kupitia ukeni na kuangalia mfuko wa uzazi na mayai ya mwanamke. Kwa kutumia kipimo hiki, ni rahisi kwa daktari kugundua kama uvimbe kwenye mayai ni wa aina gani na kujua kama ni maji tu (fluid filled sac), au ni maji pamoja na mchanganyiko wa vitu vigumu kwa maana ya complex, au ni vitu vigumu pekee ambapo huitwa completely solid.

Matibabu ya Uvimbe kwenye Mayai

Wanawake wengi wenye  vimbe ndogo ndogo lakini kwa sababu hazina dalili hahawezi kwenda hospitali. Hawa  siku wakibeba ujauzito uvimbe unaongezeka sababu ya vichocheo kuvurugika na hivyo hawa watu wabainika wanapofanyiwa ultrasound ndipo wanakutwa navyo.

Lakini kitalamu hospitali hawatibu uvimbe wa namna hii. Uvimbe ambao ni mkubwa wenyewe hutibiwa kwa namna zifuatazo (hospital)

Dawa na upasuaji

 • Vidonge vya maumivu
 • Vidonge vya kuzuia damu kama tranexamic acid na dawa za uzazi wa mpango(COCs)
 • Njia ya pili ni operation nazo zipo operation aina nyingi inategemea na uvimbe ukubwa na wingi wake.
  • Myomectomy hii ni operation ya kuondoa uvimbe mmoja mmoja bila kuondoa kizazi kwa wale wenye uvimbe mmoja uko sehemu nzuri
  • Total abdominal hysterectomy. Hii operation unaondoa kizazi chote kama uvimbe umekaa vibaya na viko vingi.

Swali la kujiuliza kwa nini mpaka upate dalili ndo utaanza kushughulikiwa kutibiwa? Kwa nini ubebe ujauzito huku una uvimbe, shughulika kwanza na tatizo kabla hujabeba ujauzito.

Share and Enjoy !

Shares
Shares