Kutokana na maoni ya watu wengi wakitaka kufahamu kuhusu tiba mbadala ya kifafa kwa watoto na wakubwa tumeamua kuandaa makala hii malumu yenye uchambuzi wa kina.
Ugonjwa wa kifafa ama seizure kwa lugha ya kitaalamu, ni ugonjwa ambao unasabababishwa na seli za mishipa ya fahamu zilizopo kwenye ubongo kutoa umeme [impulses] mwingi kuliko kawaida kwenda kwenye misuli na sehemu zingine za mwili. Na kusababisha mtu kupata dalili kama vile kuishiwa nguvu, kichwa kuuma, kuchanganyikiwa, mwili kukakamaa na hata kupoteza fahamu. Hali hii hujirudia mara kwa mara.
Ifahamike kuwa aina ya kifafa inayojulikana sana mitaani ni ile ambayo mtu anakakamaa na kupoteza fahamu. Japokuwa kuna aina za kifafa ambazo mtu hakakamai wala kupoteza fahamu, kama tutakavyoona hapo baadae.
Mgonjwa huyu huweza kuanguka mara kadhaa kwa mwezi lakini anaweza asianguke kabisa kama anafuata masharti na utaratibu mzuri wa matibabu. Mwaka 2013 ugonjwa huu uliua zaidi ya watu laki moja duniani, 80% wakiwa waafrika.
Chanzo Cha Ugonjwa Wa Kifafa Ni Nini?
Chanzo kikuu cha ugonjwa huu kwa watu wengi hua hakifahamiki lakini baadhi ni moja ya sababu za kuugia kifafa.
Kurithi; familia na koo zingine zinakua na ugonjwa huu hivyo watoto na wajukuu huzaliwa tayari na ugonjwa huu.
Kuumia kichwa: ajali zinazohusisha kuumia kwa kichwa huweza kusababisha kuumia kwa mishipa ya fahamu na mtu kuugua kifafa.
Magonjwa mengine; kuna magonjwa mtu akiugua maishani mwake baadae huweza kupata kifafa kwasababu magonjwa hayo yanavyoharibu mfumo wa ubongo.. mfano homa ya uti wa mgongo kitaalamu kama meningitis.
Uvimbe kwenye ubongo: matatizo ya uvimbe kwenye ubongo kama kansa huweza kusababisha mtu kuugua kifafa.
Kiharusi; Huu ni ugonjwa ambao husababishwa na damu kushindwa kupita vizuri kwenye ubongo au kupasuka kwa mishipa ya damu ya ubongo hali hii husababisha mtu kupooza nusu ya mwili wake na huweza kuugua kifafa baadae.
Matatizo wakati wa kuzaliwa: wakati mwingine mototo huzaliwa kwa shida sana kwa njia ya kawaida kiasi kwamba kichwa chake hubanwa sana wakati wa kupita na hali hii huweza kumsababishia kifafa kwanzia utotoni.
Matatizo ya utengenezaji wa mtoto tumboni; wakati mwingine ile miezi mitatu ya kwanza ambayo mtoto ndio anapata viungo tumboni huweza kutokea kasoro kwenye mfumo wa fahamu za kwenye ubongo na kumfanya apate kifafa akizaliwa.
Magonjwa ya uzee yanayoathiri ubongo; kuna magonjwa huharibu ubongo wakati wa uzee na magonjwa haya huweza kusababisha kifafa kipindi hicho.
Aina Za Kifafa
1)Primary generalized seizures
Hii ndio aina ya kifafa ambayo inafahamika sana mitaani; na inahusisha mgonjwa kukamaa, na kupoteza fahamu, pamoja na dalili zingine kama vile kutoa povu mdomoni, na kujisaidia haja kubwa na/au ndogo bila kujitambua akishikwa na hali hiyo.
Pia wengine hupatwa kama na wazimu au kuchanganyikiwa kwa muda kabla au baada ya kushikwa na hali hiyo.
2)Partial seizures
Aina hii ya kifafa ni ile ambayo haihusishi muhusika kupoteza fahamu na kukakamaa!! Bali hushikwa na hali fulani kama ya bumbuwazi kwa dakika kadhaa; Wengine huwa na dalili zisizoeleweka za mara kwa mara kama vile kuishiwa nguvu, kizungu zungu, kichwa kuuma sana (bila sababu ya kiafya inayojulikana), na kadhalika. Aina hizi za kifafa ziko nyingi, na dalili hutofautiana kwa kadri ya aina ya kifafa!!
Vipimo Vinavyofanyika Kugundua Ugonjwa Wa Kifafa
Ugonjwa huu unaweza kutambulika kwa daktari kuchukua historia ya dalili zinazomkabili muhusika tu(hakuna kipimo ambacho kinaweza kutambua kifafa kwa asilimia 100); Kuna kipimo kinachopima jinsi ubongo unavyotoa taarifa za umeme (ELECTROENCEPHALOGRAM-EEG), ambacho kinaweza kutambua kifafa, lakini kipimo hiki kinaweza kikaonekana kuwa hakina shida, na bado mtu akawa na tatizo hilo la kifafa. Hivyo basi, kifafa ni moja kati ya magonjwa machache ambayo kutambulika kwake kunategemea sana ujuzi na utaalamu wa daktari katika kuunganisha dalili za mgonjwa kuliko vipimo!!
Hata hivyo, mara nyingi nyingi mgonjwa hupimwa vipimo tofauti ili kuweza kujua chanzo cha ugonjwa… mfano
- Uwezo wa kufanya kazi figo
- Uwezo wa kufanya kazi maini
- Kupima maji ya uti wa mgongo
- Kupima Kaswende
- Picha ya ubongo mfano CT SCAN.
Dawa Ya Ugonjwa Wa Kifafa
Kama kawaida chanzo cha ugonjwa kikipatikana mgonjwa huanzishiwa matibabu lakini kama mgonjwa alikua tayari ameshapata madhara kwenye ubongo kulingana na chanzo husika ataendelea kua na kifafa lakini makali yake hupungua kadiri anavomeza dawa.
Matibabu yasiyo ya dawa wakati mgonjwa amekamatwa na kifafa:{non pharmacological treatment}
- Mzuie mgonjwa asijiumize kwa kuweka kitu laini chini ya kichwa chake, ondoa vitu vikali karibu yake kama kisu, sindano au vyuma.
- Usilazimishe kitu chochote kwenye mdomo wa mgonjwa.
- Usimshike kuzuia mizunguko yake
- Weka kichwa alale anaangalia upande mmoja ili kutoa mate mdomoni.
- Kaa na mgonjwa mpaka degedege ziishe
- Usiweke chochote mdomoni kwa mgonjwa kama dawa au chakula mpaka apate fahamu zake.
Dalili Za Mtu Mwenye Kifafa
kwa mtu mwenye kifafa hali hii ya kukamatwa na degedege za kifafa sio ya ajabu sana ila ukiona dalili hizi mkimbize hospitali..
- Degedege za kifafa zaidi ya dakika kumi
- Kutapika sana
- Kushindwa kuona vizuri
- Kupoteza fahamu
- Kichwa kuuma sana.
Matibabu Kwa Mgonjwa Wa Kifafa.
Mgonjwa akishagundulika na kifafa ataanzishiwa dawa kama carbamizapine, phenorbabitone au zingine za kifafa na atakua anameza kila siku ili kuzuia hali hiyo ya kuanguka na kupoteza fahamu na akifuata masharti ataishi maisha ya kawaida kabisa.
Mambo Yanayofanya Kupata Degedege Za Kifafa Mara Kwa Mara
- Kukosa usingizi kwa muda mrefu
- Mianga na miale ya disco
- Unywaji wa pombe
- Kuishiwa sukari mwilini wakati wa akisikia njaa kali.
- Kutomeza dawa kama ilivyoelekezwa
NB. Hatuna dawa za kutibu kifafa, hivo mgonjwa apelekwe hospitali ya karibu